Riwaya ya Shamba la wanyama
(1945), ni moja kati ya kazi nzuri kabisa za kibunifu katika Tasnia ya fasihi
andishi hapa duniani. Riwaya hii ambayo iliandikwa na Muingereza ambaye ni maarufu
kwa jina la George Orwell, ni mtiririko wa sitiari (allegory) unaoakisi dhana
nzima ya ujamaa wa kidemoskrasia katika tawala mbali mbali za kidunia.
Kazi hii yenye ubora, ladha na
mvuto usiochosha, inahusu kisa cha dola la wanyama. Wanyama ambao kwa pamoja
walikubaliana kuungana na kuishi kwa misingi ya usawa na haki. Moja kati ya
kanuni hizo za usawa, ilikubaliwa kwamba hakuna mnyama mmoja atakemdhuru mnyama
mwengine ama kwa kumla, kumpiga, kumdhulumu na hata kumuuwa. Kanuni hii ilipita
na ikaandikiwa kauli mbiu (slogan) isemayo ‘Wanyama wote ni sawa’!
Kwa muda baada ya kanuni hii
kupitishwa na kukubaliwa na wanyama wote, wanyama wadogo wadogo na wale
waliokuwa waathirika wa vitimbi, viteweji na mateso ya wanyama wakubwa,
walihisi kupata faraja kubwa kwa kuhakikishiwa usalama wao. Imani yao hii
ilichangiwa na kuona kauli ile mbiu ikiimbwa na kuandikwa kila kona ya dola lao
lile kiasi ya kumfanya kila mnyama aamini kile anachokiona katika kauli mbiu
ile.
Waswahili husema ‘Taa haachi
mwiba wake’. Haikutimia wiki, kuna baadhi ya wanyama hasa ndege, walianza kuona
dalili mbaya katika jamii yao. Moja ya dalili hio ni kupotea kwa baadhi ya
wanyama katika mazingira ya kutatanisha. Kwa lugha nyepesi, kuna baadhi ya
wanyama walianza kuwala wengine kimya kimya kila siku.
Wanyama wadogo walipogundua
usaliti huu walirudi kwa mkubwa wao kushitaki na kusimulia masikitiko yao juu
ya kitendo hiki cha uvunjifu wa amani, na usalama wa wanyama katika dola yao.
Kwa bahati mbaya walipofika mahala pa mashtaka na kueleza makosa yao, waliona
ile kauli mbiu imebadilishwa kidogo kutoka ilivyokuwa mwanzo.
Awali kauli ilisomeka ‘Wanyama
wote ni sawa’, lakini sasa inasomeka ‘Wanyama wote ni sawa, lakini baaadhi ya
wanyama, ni sawa zaidi kuliko wengine’! Kisa hichi kikaishia hapo. Kumalizika
kwa kisa hiki ndipo tunapopata nadharia hiyo niliyoitumia katika kichwa cha
makala hii hapo juu, ambayo ni moja ya nadharia maarufu duniani kwa sasa. Yaani
nadharia ya ‘Ki-Orwelli’.
Nimewajibikiwa na kuandika kwa
kusema kuwa kwa namna mchakato mzima wa maoni ya katiba unavyokwenda, nanusa
harufu ile ile waliyoinusa wanyama wadogo kama mimi katika ‘Shamba la wanyama’.
Harufu ya kwamba kuna baadhi ya wanyama ni sawa kuliko wengine. Na hii si
tuhuma kutoka katika ombwe la uwazi, bali ina kila aina ya ithibati na
visherehesho vya kuutilia shaka mapema mchakato huu wa katiba nchini.
Nilitegemea iwapo maoni ya katiba yalilenga kukusanya maoni ya
wananchi, kwa haki na usawa, na ili yanipe imani kuwa haki itatendeka, basi
yalikuwa yafanywe kwa wanachi wote bila kuweka tabaka (strata/ social classes).
Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika mchakato wa katiba, wananchi wote, wake
kwa waume, wakubwa kwa wadogo, viongozi na waongozwa, mashehe na mapadiri,
wanasiasa na majeshi, wote kwa pamoja ni wananchi walio sawa. Na mchakato wa katiba
ulikuwa uanze na kauli mbiu hiyo ya ‘ Wananchi wote ni sawa mbele ya haki na
sheria’!
Kuwe na usawa kwamba, maoni ya
katiba yafanyike kama vile tunavyofanya uchaguzi. Yapitie kimajimbo au maeneo
ya ukazi wa wananchi. Sasa maoni yakifika jimbo ambalo kiongozi mkuu wa nchi au
mstaafu anapoishi, basi hio ndio iwe
zamu yake ya kwenda kutoa maoni hapo kwao. Kwa mfano, ikiwa Rais wa Zanzibar
anaishi Mbweni, basi maoni yakifika jimbo la eneo hilo, iwe ndio zamu yake ya
kutoa maoni na wananchi sawia, ijapokuwa atapewa nafasi ya kwanza kufanya
hivyo, lakini utaratibu uwe hivyo.
Na nilitegemea iwe hivi kwa watu
wote nchi nzima. Wa Bagamoyo akatowe
maoni kwao, alie Dar es Salaam atatoa maoni hapo jimboni kwake, alie kambini kwa jeshi bila shaka kambi hio haiko
angani, aende jimbo ilipo kambi hio akatoe maoni. Na kwa mpangilio kama huu
angalau tungeweza kuamini kwamba mchakato wa katiba una sura ya usawa na hivyo
haki haichezi mbali.
Lakini ni jambo la kushangaza
sana kuona tume ya Katiba inapitia majumbani mwa viongozi na wastaafu, wizara,
idara, na mashirika ya Serikali, na halafu pengine hata taasisi za kidini, ili
kukusanya maoni. Utaratibu huu unaleta
matabaka kwa wananchi. Na asili na maumbile ya mfumo wa kitabaka duniani dumu
daima hautendi haki. Huu ndio uhalisia wa nadharia na mifumo yote ya kitabaka
duniani.
Kwa mujibu wa mwenendo wa
mchakato huu wa katiba unavyoendeshwa, wa kuanza kijumba hodi, unaonesha wazi
kuwagawa wananchi na kuwafanya wasiwe sawa mbele ya haki. Binadamu ni mtu
aliemumbwa na fikra, akili, na maarifa.
Unapomleta mtu kama Mkapa jimboni kutoa
maoni na wanachi wengine, hata akizomewa, watu watahisi kuwepo kwa usawa. Na
unapompa siku yake pekee tena nyumbani kwake, unaanza kuuumba dudu moja baya
mno la ubaguzi na ngazi refu ya utabaka baina ya wananchi na wakubwa wao.
Taswira inayojengeka machoni mwa
wananchi hivi sasa, kwa tume kuanza kupitia watu binafsi majumbani kukusanya
maoni yao, eti tu kwa sababu ni wakubwa,
haina mustakabali mzuri. Haina kwa sababu tafsiri iko wazi ya utaratibu kama
huu. Iko wazi hata kwa kujiuliza swali dogo tu. Hivi kweli maoni waliyotoa
wananchi wote wa Zanzibar, yanawezajae kuyapindua maoni aliyoyatoa Mkapa na
Mwinyi? Sipati picha!
Yaani, hivi kweli maoni ya wananchi
wa kawaida yatasikilizwa bora kwa kulinganisha wingi wao kuliko ukubwa na maoni
ya wenye cheo, kauli, na nguvu katika nchi hii? Hili si kweli, maana tumeona
katika chaguzi nyingi hapa nchini, ambapo sauti ya wananchi walio wengi
ikipinduliwa na kauli ya mtu mmoja. Hili liko wazi kama sabuni ya mche!
Na ndio hapa ninapoona kuwa ile
kauli mbiu isemayo ‘Watu wote ni sawa mbele ya haki na Sheria’ ikibadilika na
kusomeka ‘Watu wote ni sawa mbele ya haki na sheria, lakini baadhi ya watu, ni sawa zaidi kuliko wengine’. Kwa hali hii
naanza kukosa imani na kutawaliwa na ruwaza za nadharia ya ‘Ki-Orwell’
ninapautazama mchakato mzima wa katiba hapa nchini unavyokwenda.
Natoa hoja.
(Imechapishwa kutoka mtandao wa Mzalendo.net)